1 Thessalonians 5

Kuweni Tayari Kwa Siku Ya Bwana

1 aBasi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia, 2 bkwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku. 3 cWakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.

4 dBali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi. 5 eNinyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. 6 fKwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. 7 gKwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. 8 hLakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. 9 iKwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Isa Al-Masihi. 10 jYeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye. 11 kKwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.

Maagizo Ya Mwisho, Salamu Na Kuwatakia Heri

12 lSasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya. 13 mWaheshimuni sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi. 14 nNasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote. 15 oAngalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

16 pFurahini siku zote; 17 qombeni bila kukoma; 18 rshukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Al-Masihi Isa.

19 sMsiuzime moto wa Roho Mtakatifu; 20 tmsiyadharau maneno ya unabii. 21 uJaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema. 22 vJiepusheni na uovu wa kila namna.

23 wMungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Isa Al-Masihi. 24 xYeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.

25 yNdugu, tuombeeni. 26Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu. 27Nawaagizeni mbele za Bwana mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii.

28Neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe nanyi. Amen.
Copyright information for SwhKC